Sunday, August 18, 2013

Jongoo mjinga na Nyoka mjanja

SIKU moja mama yake Jongoo alimtuma mwanawe kwenda kumsabahi baba yake Mama Jongoo, yaani, Babu yake Jongoo. Wakati huo Jongoo alikuwa na macho mawili, lakini hakuwa na miguu kama alivyo hivi leo. Njiani Jongoo alikutana na Nyoka. Nyoka alikuwa na sifa ya kuwasifia na kuwapamba watu vilivyo, na hasa alipokuwa kuna kitu anahitaji kupata kutoka kwa msifiwa. Alimsifia Jongoo alivyokuwa na ngozi mororo na laini, na kisha macho yake yalivyokuwa mweupe na mwendo wake wa madaha. Sifa hizi zikamwiingia Jongoo kichwani. Kichwa kikavimba sana. Kisha Nyoka chapuchapu akacheza karata yake. Akamwambia Jongoo kwamba anaomba amuazime macho yake kwa angalau masaa machache ili aende akamuone Binti Nyoka anayekwenda kumchumbia ambako huko pia kulikuwa na nogma ya yeye kwenda kuposa. Jongoo alisita kwa muda. Hata hivyo, Nyoka alizidi kumbembeleza na kumpa miguu yake kama rehani. Kuona hivi Jongoo akakubali kumuazima macho yake Nyoka. Do, Nyoka alipofika na kumuona binti yule alivyo mzuri, hakutaka tena kurudisha macho na kukosa starehe kama ile. Aidha, ngoma na shamrashamra zilivyopendeza ndiyo zikazidi kumtia husuda na inda na akaamua kutomrudishia Jongoo macho yake, pamoja na kususa miguu yake mingi aliyomwachia Jongoo. Baada ya Baba na Mama Jongoo kumtafuta mtoto wao hadi kwa Babu yake na kumkosa huko, waliamua kuripoti kwa Chifu. Ikapigwa baragumu na watu wakaenda kumsaka Mwana Jongoo. Walimkuta porini hali kipofu akihangaika nusura ya kutumbukia baharini. Fundisho: 1. Usiazime unachokithamini sana, utakuja lijutia. 2. Epuka watu wanaokusifu, kisha jali wanaokukosoa!

Mamba na nyani walivyokosana

KILA asubuhi mamba alikuwa akivuka mto toka upande aliokuwa akilala kwenda upande alikokuwa akishinda na kuwinda. Aghalabu, mgongoni mwake siku zote kulikuwa na abiria mmoja. Abiria huyu alikuwa nyani. Nyani hakupenda kuguswa na maji hata siku moja.Ndiyo sababu akamuomba Mamba awe anampanda mgongoni kwake kila anapovuka asubuhi na kurejea nyumbani jioni. Pamoja na ukarimu huu wa mamba, nyani hakuwa na shukrani. Kila akikaa juu ya mgongo wa mamba pakiwa na mtu mwingine, alikuwa na tabia ya kumkashifu Mamba. Alisema akinong'oneza, kwamba Mamba ni mchafu, mgongo wake unanuka na umejaaa tope na takataka. Mamba alipouliza Nyani anazungumzia nini, Nyani alijibu haraka haraka na kusema tunakusifia kwa jinsi unavyochanja mbuga majini. Wewe bwana unajua kuogelea sana. Hata hivyo, siku moja Sungura alimtobolea Mamba siri ya kukashifiwa, lakini kwa undumilakuwili wake pia akamwambia Nyani kwamba atakiona akipanda tena mgongoni kwa Mamba, kwa kuwa yeye, Sungura, keshamwambia Mamba kashifa anazotoa akiwa mgongoni mwake. Siku ambayo Mamba aliamua kumtia adabu mbata wake, Nyani, hakuwa na furaha kabisa. Nyani akahisi kuwa Mamba ana lake jambo. Akawa katika hali ya tahadhari. Walipokuwa wanakaribia ng'ambo ya pili Mamba alitaka kupiga mbizi ili kumkamata Nyani kwa urahisi. Hata hivyo, Nyani alidaka tawi la mti lililokuwa karibu naye, na huyo akakwea juu na kuepuka adhabu yake. Mamba akamwambia:" Ole wako, ukikaa tena juu ya mgongo wangu au ukikanyaga maji mahala nilipokaa maana huo utakuwa ndiyo mwisho wako. Fundisho: Neno moja tu linaweza kuvunja urafiki uliodumu kwa muda mrefu.

Sunday, March 15, 2009

Mbweha na Mbuzi

Mbweha alikuwa akitafuta chakula nyikani wakati alipomuona mbuzi kileleni juu ya mwinuko
akila majani.

Kwa kuwa mwenyewe alikuwa hawezi kupanda kule juu alifikiria namna ya kufanya mbuzi ateremke na kuja chini ili amle.

Akamwita mbuzi na kumwambia:
"Samahani mwenzangu mbuzi," akasema kwa sauti ya upole," ni hatari sana kukaa mahala kama hapo ulipo. Shuka chini kabla hujaumia. Isitoshe majani hapa chini ni laini na matamu zaidi kuliko hayo ya huko juu. Sikiliza ushauri wangu na ushuke chini kwa usalama wako."

Hata hivyo mbuzi alimfahamu mbweha fika na nia yake mbaya.

"Nenda zako hayawani wee. Haujali chochote kuhusu usalama wangu. Na wala hujali kama ninakula majani mazuri au mabaya. Nia yako ni kutaka mimi nishuke ili unile tu! Umefulia leo! Ishilia zako!"

Adili au somo la hadithi: Kuwa na mashaka na ushauri 'mzuri' toka kwa adui yako.
Hafeez Sammy na Shukrani: Simulizi za Aesop.