Sunday, August 18, 2013

Jongoo mjinga na Nyoka mjanja

SIKU moja mama yake Jongoo alimtuma mwanawe kwenda kumsabahi baba yake Mama Jongoo, yaani, Babu yake Jongoo. Wakati huo Jongoo alikuwa na macho mawili, lakini hakuwa na miguu kama alivyo hivi leo. Njiani Jongoo alikutana na Nyoka. Nyoka alikuwa na sifa ya kuwasifia na kuwapamba watu vilivyo, na hasa alipokuwa kuna kitu anahitaji kupata kutoka kwa msifiwa. Alimsifia Jongoo alivyokuwa na ngozi mororo na laini, na kisha macho yake yalivyokuwa mweupe na mwendo wake wa madaha. Sifa hizi zikamwiingia Jongoo kichwani. Kichwa kikavimba sana. Kisha Nyoka chapuchapu akacheza karata yake. Akamwambia Jongoo kwamba anaomba amuazime macho yake kwa angalau masaa machache ili aende akamuone Binti Nyoka anayekwenda kumchumbia ambako huko pia kulikuwa na nogma ya yeye kwenda kuposa. Jongoo alisita kwa muda. Hata hivyo, Nyoka alizidi kumbembeleza na kumpa miguu yake kama rehani. Kuona hivi Jongoo akakubali kumuazima macho yake Nyoka. Do, Nyoka alipofika na kumuona binti yule alivyo mzuri, hakutaka tena kurudisha macho na kukosa starehe kama ile. Aidha, ngoma na shamrashamra zilivyopendeza ndiyo zikazidi kumtia husuda na inda na akaamua kutomrudishia Jongoo macho yake, pamoja na kususa miguu yake mingi aliyomwachia Jongoo. Baada ya Baba na Mama Jongoo kumtafuta mtoto wao hadi kwa Babu yake na kumkosa huko, waliamua kuripoti kwa Chifu. Ikapigwa baragumu na watu wakaenda kumsaka Mwana Jongoo. Walimkuta porini hali kipofu akihangaika nusura ya kutumbukia baharini. Fundisho: 1. Usiazime unachokithamini sana, utakuja lijutia. 2. Epuka watu wanaokusifu, kisha jali wanaokukosoa!

1 comment: