Sunday, August 18, 2013

Mamba na nyani walivyokosana

KILA asubuhi mamba alikuwa akivuka mto toka upande aliokuwa akilala kwenda upande alikokuwa akishinda na kuwinda. Aghalabu, mgongoni mwake siku zote kulikuwa na abiria mmoja. Abiria huyu alikuwa nyani. Nyani hakupenda kuguswa na maji hata siku moja.Ndiyo sababu akamuomba Mamba awe anampanda mgongoni kwake kila anapovuka asubuhi na kurejea nyumbani jioni. Pamoja na ukarimu huu wa mamba, nyani hakuwa na shukrani. Kila akikaa juu ya mgongo wa mamba pakiwa na mtu mwingine, alikuwa na tabia ya kumkashifu Mamba. Alisema akinong'oneza, kwamba Mamba ni mchafu, mgongo wake unanuka na umejaaa tope na takataka. Mamba alipouliza Nyani anazungumzia nini, Nyani alijibu haraka haraka na kusema tunakusifia kwa jinsi unavyochanja mbuga majini. Wewe bwana unajua kuogelea sana. Hata hivyo, siku moja Sungura alimtobolea Mamba siri ya kukashifiwa, lakini kwa undumilakuwili wake pia akamwambia Nyani kwamba atakiona akipanda tena mgongoni kwa Mamba, kwa kuwa yeye, Sungura, keshamwambia Mamba kashifa anazotoa akiwa mgongoni mwake. Siku ambayo Mamba aliamua kumtia adabu mbata wake, Nyani, hakuwa na furaha kabisa. Nyani akahisi kuwa Mamba ana lake jambo. Akawa katika hali ya tahadhari. Walipokuwa wanakaribia ng'ambo ya pili Mamba alitaka kupiga mbizi ili kumkamata Nyani kwa urahisi. Hata hivyo, Nyani alidaka tawi la mti lililokuwa karibu naye, na huyo akakwea juu na kuepuka adhabu yake. Mamba akamwambia:" Ole wako, ukikaa tena juu ya mgongo wangu au ukikanyaga maji mahala nilipokaa maana huo utakuwa ndiyo mwisho wako. Fundisho: Neno moja tu linaweza kuvunja urafiki uliodumu kwa muda mrefu.

2 comments:

  1. wasomaji wa kazi zako tupo endelea kupost. tupo na tunasubiri kazi zako.

    ReplyDelete
  2. Hii hadithi ni ya kusisimua. Pongezi.

    ReplyDelete